USB OTG ni nini? Je simu yako ina #teknolojia hii?

Teknolojia ya USB ni moja ya teknolojia zinazotumika zaidi katika suala zima la uhamishaji wa mafaili na uunganishwaji wa vifaa tofauti tofauti vya elektroniki. USB OTG inakuwezesha kuunganisha vitu kama USB Flash Drive, keyboard n.k na simu yako.

USB On-The-Go (OTG) ni mfumo wa kielektroniki unaoruhusu vifaa vya elektroniki ambavyo si kompyuta kuweza kusoma data kutoka vifaa vingine vya elektroniki bila uhitaji wa kompyuta.
Waya (cable) wa USB OTG – Upande mmoja unaweza chomekwa kwenye simu au tableti alafu upande wa pili unaweza tumiwa kuchomekwa keyboard, kipanya au kifaa kingine chochote cha elektroniki kwa njia ya USB

Mambo yanayowezekana kutokana na teknolojia ya USB On-The-Go

Unaweza kusoma data kama vile miziki, video na mafaili mengine kutoka kwenye USB Flash Drive.
Pia unaweza tumia ‘Vichezea Magemu’, yaani ‘Game controllers’ kimombo ili kuweza kucheza magemu ya kwenye simu janja au tableti yako kwa urahisi.

Je kifaa chako kina teknolojia ya USB OTG

Ingawa teknolojia hii inawezekana kwenye vifaa vingi vya kisasa vya Android (simu na tableti) pia inaweza tumika kwenye vifaa vingine mbalimbali kama vile baadhi ya simu za Windows. Hadi sasa hakuna dalili ya Apple kuiruhusu katika simu zao za iPhone.
Pia simu na tableti nyingi za kisasa zilizotoka katika kipindi cha miaka miwili hivi zimekuja na teknolojia hiyo.

Njia nyingine kwa watumiaji wa simu za Android ni kupakua app ya USB OTG Checker. App hii inasaidia kuitambua simu yako na programu endeshaji yake na kisha kukuambia kama simu hiyo imekuja na uwezo huo – USB OTG.

Je vifaa vya USB OTG unaweza vipata wapi?

Unaweza nunua ‘cable’ za USB OTG kwenye maduka ya elektroniki, si yote yanaweza kuwa nayo ila tayari zinapatikana kwenye maduka mengi. Uangaliaji wetu wa haraka haraka kwenye mtandao wa mauzo ya kimtandao – Jumia tumeweza kuona zinapatikana.

Pia tayari kuna USB Flash diski zinazokuja na teknolojia ya USB OTG upande wa pili na hivyo zinaweza kuchomekwa kwenye simu na mtu kuweza kuhamisha mafaili moja kwa moja kutoka kwenye flashi diski hiyo kwenda kwenye simu n.k.

Je wewe ushawahi kutumia teknolojia hii? Tuambie maoni yako.

Comments :

Post a Comment

write to us your views on this

Interested to get more of our Update !